MASWALI NA MAJIBU
TSA NI NINI?
Tanzania Sharing Association ni kikundi cha watanzania waishio nchini Marekani. Kikundi hiki kilianzishwa jijini Houston, Texas kwa lengo la kujenga umoja, ushirikiano, na kusaidiana katika shida na raha. Hivi sasa kikundi kina wanachama kutoka majimbo (states) yote ya Marekani.
SIFA ZA KUWA MWANACHAMA NI ZIPI?
Mtu yeyote mwenye asili, au nasaba ya kitanzania kwa kuzaliwa, kuoa au kuolewa, au kuandikishwa anaruhusiwa kuomba uanachama wa TSA. Hata hivyo, kabla ya kujiunga muhusika hutakiwa kujaza fomu ya maombi na baadae kujadiliwa na kamati maalum ya kikundi kuthibitisha sifa na mwenendo wao. Wanachama wanayo haki ya kikatiba kumkataa mtu yeyote anayeomba uanachama endapo watabaini anaweza kuleta matatizo, au kuvuruga maslahi ya kikundi.
NINI FAIDA YA KUWA MWANACHAMA?
Mwanachama wa TSA hufaidika kwa namna nyingi kutokana na upendo, ushirikiano, na msaada wa kipekee unaotolewa na wanachama wenzie katika kundi. Mwanachama akifariki, kikundi hugharimia sehemu ya mazishi yake kwa kutoa $10,000. Kiasi hicho pia hupewa mwanachama endapo atafiwa na mtoto hapa Marekani. Vilevile mwanachama husaidiwa $3,000 endapo akifiwa na mzazi au mlezi wake aliye mahali popote duniani, au akipatikana na janga lingine kama ugonjwa wa muda mrefu, au kuunguliwa moto nyumba.
VIONGOZI WA TSA HUPATIKANAJE?
Viongozi wa TSA hupatikana kwa kupiga kura. Kila mwanachama hai ana haki ya kupiga kura kuchagua viongozi, na pia kugombea nafasi ya uongozi iliyo wazi. Viongozi wanaochaguliwa hufanya kazi kwa kujitolea, hawalipwi mshahara.
KUNA ADA YA KIINGILIO?
Mwanachama mpya hutakiwa kulipa ada ya $225. Kati ya hizo $100 ni tozo la kiingilio, $25 ni ada ya mwaka, na $100 ni mchango unaoingizwa kwenye mfuko wa kikundi. Pamoja na ada hiyo mwanachama mpya huwekwa katika uangalizi (probation) wa siku 60. Katika kipindi hicho mwanachama hastahili kulipwa mafao yoyote, bali wanachama huweza kumpa mchango wa hiari (Rejea katiba). Mwanachama ataweza kupokea mafao baada ya kuvuka kipindi cha matazamio.
JE! MWANACHAMA ANAWEZA KUJITOA KATIKA KUNDI?
Mwanachama anao uhuru wa kujitoa katika kikundi (kujivua uanachama) muda wowote anaotaka endapo atakuwa hajawahi kupokea mafao. Mwanachama aliyepokea mafao atapaswa kurudisha pesa aliyolipwa kabla ya kujitoa. Utaratibu huu umewekwa kikatiba kwa lengo la kulinda fedha na mali za TSA. Aidha, wanachama wa TSA wanayo haki ya kikatiba kumvua uanachama mtu yeyote atakayeonekana kuhatarisha usalama au maslahi ya kikundi. Kwa ufafanuzi tafadhali soma katiba ya Tanzania Sharing Association.
BOFYA HAPA CHINI KUSOMA KATIBA YA TSA
